Friday, March 28, 2014

Yanga ndani ya Tanga tayari kwa mechi ya kesho

MABINGWA watetezi wa Ligi Kuu ya soka ya
Tanzania Bara, Yanga wamewasili jijini Tanga
jana tayari kuvaana na Mgambo JKT katika
mchezo utakaopigwa kesho kwenye Uwanja
wa Mkwakwani.
Kwa mujibu wa Ofisa Habari wa Yanga, Baraka
Kizuguto, wamewasili salama mkoani humo, ila
alisema hana taarifa za benchi la ufundi
kuhusu hali za wachezaji katika mechi hiyo.
Hata hivyo, Yanga haina majeruhi wapya kwa
siku za karibuni kwani kikosi chake chote kiko
imara na hiyo ni muhimu hasa wakati huu
inapoifukuzia Azam FC katika kuwania ufalme
wa soka Tanzania Bara.
Mabingwa hao watetezi wako nyuma ya Azam
FC kwa pointi nne, lakini wakiwa na mchezo
mmoja mkononi, hivyo pointi tatu ni muhimu
kwao.
Yanga inaikabili Mgambo JKT ikiwa na
kumbukumbu nzuri ya kutoka kuibugiza
Tanzania Prisons kwa mabao 5-0 kwenye
Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, hivyo iko
vizuri kisaikolojia.
Wapinzani wao, Mgambo JKT wametoka
kuchapwa mabao 2-0 na wapinzani wakubwa
wa Yanga, Azam FC kwenye uwanja huo wa
Mkwakwani, Jumatano wiki hii, hivyo wataingia
uwanjani kesho kama simba aliyejeruhiwa, na
hasa ikitiliwa maanani ligi inaelekea ukingoni,
na haitaki kushuka daraja.
Mgambo ni timu ambayo iko katika hatari ya
kushuka daraja kwani iko nafasi ya 11 ikiwa na
pointi 19, inaweza kutumia uwanja wake wa
nyumbani kutoka sare au ushindi hivyo Yanga
wana kibarua kizito.
Kwa upande wake, kesho Azam itavaana na
Simba yenye pointi 36 ikiwa nyuma kwa pointi
11 na ambayo imekuwa ikifanya vibaya katika
baadhi ya mechi zake.
Simba ni timu isiyotabirika inaweza ikafanya
vizuri ili wasibaki nyuma ingawa Azam pia, ni
timu inayotumia mashambulizi ya kushtukiza.
Katika mbio za kusaka ubingwa baada ya
kuvaana na Simba, bado Azam itakuwa na
kibarua kizito kwa Mbeya City, ambayo ina
kumbukumbu ya kupoteza mechi moja katika
Uwanja wa Sokoine.
Mechi nyingine zitakazochezwa kesho ni
Mbeya City dhidi ya Tanzania Prisons (Mbeya),
Kagera Sugar dhidi ya Ruvu Shooting (Kaitaba)
na Mtibwa Sugar itakuwa ni mwenyeji wa
Coastal Union (Manungu) wakati JKT Ruvu
itavaana na Rhino Rangers kwenye Uwanja wa
Azam Complex, Chamazi Dar es Salaam.
Ligi hiyo itaendelea leo kwa Ashanti United
kukabiliana na JKT Oljoro kwenye Uwanja wa
Azam Complex. Timu hizo zote ziko kwenye
hatari ya kushuka daraja, katika msimamo wa
ligi, Ashanti United ina pointi 18 wakati Oljoro
ina pointi 13. Ni tofauti ya pointi tatu.

No comments:

Post a Comment