Sunday, March 23, 2014

AZAM FC MAMBO SAFI....SIMBA HOI...

AZAM FC imezidi kutakata kileleni mwa
msimamo wa Ligi Kuu ya soka ya Tanzania
Bara kwa kupata ushindi dhidi ya Oljoro JKT
wakati Simba hali yake inazidi kwenda mrama
baada ya kuzamishwa nyumbani na Coastal
Union ya Tanga.
Kwa ushindi wa bao 1-0 dhidi ya maafande
hao wa Arusha, Azam FC imefikisha pointi 47
na kuiacha Yanga nyuma kwa pointi nne,
ingawa mabingwa hao watetezi wana mchezo
mmoja mkononi.
Kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam,
Simba ilizidi kujiweka katika wakati mgumu
msimu huu na huenda ikakosa hata nafasi ya
tatu kufuatia kipigo cha bao 1-0 ilichokipata
kutoka kwa Coastal Union.
Vijana wa Msimbazi waliuanza mchezo huo
kwa kasi na kupoteza nafasi nyingi kipindi cha
kwanza kupitia kwa washambuliaji Amis
Tambwe, Ramadhani Singano, Haruna
Chanongo na kiungo wake Jonas Mkude.
‘Wagosi wa Kaya’ Coastal Union iliwabidi
kusubiri hadi dakika ya 45 kujipatia bao pekee
lililofungwa na Hamadi Juma aliyewalamba
chenga walinzi wa Simba, Donald Mosoti na
Joseph Owino kisha kupiga shuti lililompita
makwapani kipa Ivo Mapunda na kutinga
wavuni.
Katikati ya kipindi cha kwanza, Kocha Mkuu
wa Simba, Zdravko Logarusic alimtoa nje
kiungo mkongwe Henry Joseph kutokana na
kutoridhishwa na kiwango chake na
kumwingiza Said Ndemla.
Kipindi cha pili, Simba ilifanya mabadiliko kwa
kumtoa beki wa kushoto Omari Salum na
kumwingiza William Lucian aliyeipa uhai timu
hiyo kwa kupiga krosi nyingi kwenye lango la
wapinzani wao, lakini washambuliaji
walishindwa namna ya kumfunga kipa
chipukizi wa Coastal Union, Fikiri Selemani.
Coastal Union ambayo iliwachezesha
wachezaji wengi wa kikosi cha vijana,
walionekana kutulia na kutengeneza
mashambulizi yao kwa umakini kupitia kwa
Daniel Lyanga na Kenneth Masumbuko, ambao
walionekana kuisumbua ngome ya Simba mara
kwa mara, lakini hakufunga bao jingine.
Dakika tano za mwisho Simba ilionekana
kupania kusawazisha bao hilo baada ya
kufanya mashambulizi mengi kwenye lango la
Coastal Union, lakini kipa Seleman aliibuka
nyota wa mchezo baada ya kumdhibiti Singano
kufunga bao katika dakika ya mwisho ya
mchezo.
Baada ya filimbi ya mwisho, Singano alikwenda
kuvunja kioo cha mlango wa kuingilia kwenye
vyumba vya kubadilishia nguo, hivyo Jeshi la
Polisi kulazimika kumsubiri ili kumpeleka
kituoni kwa maelezo zaidi.
Kwa matokeo hayo, Simba imebaki katika
nafasi ya tatu ikiwa na pointi zake 36, pointi
sita nyuma ya wanaoshika nafasi ya tatu
Mbeya City, pointi saba nyuma ya Yanga na
pointi 11 nyuma ya vinara.
Kwenye Uwanja wa Azam Complex, Chamazi
wenyeji Azam FC walijipatia bao la ushindi
katika dakika ya 71 lililofungwa na John Bocco
kutokana na pasi ya chipukizi Kelvin Friday.
Katika mechi nyingine, Ruvu Shooting iliichapa
Ashanti United kwa mabao 2-0 kwenye
Uwanja wa Mabatini, Mlandizi mkoani Pwani.
Mabao hayo yalifungwa na Elias Maguli dakika
za sita na 63.
Ruvu imefikisha pointi 31 baada ya mechi 22
katika nafasi ya sita wakati Ashanti ni ya 12 na
pointi zake 19. Jijini Tanga, wenyeji Mgambo
JKT walilazimishwa sare ya bao 1-1 na
Mtibwa Sugar kwenye Uwanja wa CCM
Mkwakwani.
Mgambo imebaki nafasi ya 11 ikiwa na pointi
19 kwa mechi 21, wakati Mtibwa Sugar inabaki
nafasi ya nane kwa pointi zake 27 baada ya
mechi 22.
Ligi hiyo itaendelea keshokutwa Jumatano kwa
mechi kati ya Yanga dhidi ya Tanzania Prisons
kwenye Uwanja wa Taifa na Mgambo JKT
dhidi ya Azam FC kwenye Uwanja wa
Mkwakwani.

No comments:

Post a Comment