BODI ya Ligi Kuu Tanzania Bara imeitoza faini
klabu ya Simba pamoja na mshambuliaji wake
nyota, Amisi Tambwe, kutokana na makosa
mbalimbali ikiwemo vitendo vinavyoashiria
ushirikina uwanjani.
Akizungumza na waandishi wa habari jana,
Ofisa Habari na Mawasiliano wa Shirikisho la
Soka Tanzania (TFF), Boniface Wambura
alisema Simba ilifanya vitendo hivyo katika
mechi yake dhidi ya Mbeya City, na kutozwa
faini ya Sh 500,000.
Aidha, imetozwa faini ya Sh 500,000 kwa
makocha wake Zdravko Logarusic, Selemani
Matola na Idd Pazi, kwa kuingia uwanjani na
kumzonga mwamuzi kwenye mechi hiyo
kwenye Uwanja wa Sokoine, Mbeya.
Naye mshambuliaji wa Simba, Tambwe
ametozwa faini ya Sh 500,000 kwa kushangilia
bao alilofunga kwenye mechi hiyo kwa
kuonesha ishara ya matusi kwa kidole.
Wakati huo, Mbeya City imepigwa faini ya Sh
300,000 kwa mashabiki wake kuingia uwanjani
kwenye mechi dhidi ya Kagera Sugar
iliyochezwa mjini Bukoba.
Wambura alisema pia klabu za Yanga na
Coastal Union zimepigwa faini ya Sh 500,000
kila moja kwa mashabiki wao kurusha chupa
za maji uwanjani wakati timu hizo
zilipopambana jijini Tanga.
Aidha, kiungo wa Mtibwa Sugar, Shabani Nditi
amepigwa faini ya Sh 500,000 kwa kumpiga
mchezaji wa Simba, wakati Salvatory Ntebe
pia wa Mtibwa Sugar amepigwa faini ya Sh
500,000 kwa kumtukana mwamuzi kwenye
mechi dhidi ya Mbeya City.
Wambura alisema adhabu nyingine ni kwa
mshambuliaji wa Mtibwa Sugar, Musa Hassan
‘Mgosi’ ambaye amepigwa faini ya Sh 500,000
kwa kosa la kupigana uwanjani kwenye mechi
dhidi ya Ashanti United ambapo vilevile
atakosa mechi tatu za ligi.
Coastal Union imetozwa faini nyingine ya Sh
500,000 kwa mashabiki wake kumrushia
chupa za maji kipa wa Mbeya City, wakati JKT
Ruvu imepigwa faini ya Sh 300,000 kwa
kuchelewa kufika uwanjani kwenye mechi dhidi
ya Simba iliyochezwa Uwanja wa Taifa, Dar es
Salaam.
Vilevile wamiliki wa Uwanja wa Mkwakwani
jijini Tanga wameandikiwa barua ya kufanya
marekebisho ya vyumba vya wachezaji, kwa
vile havina hewa ya kutosha.
Kwa upande wa Ligi Daraja la Kwanza, klabu
zilizopigwa faini kutokana na makosa
mbalimbali ni Friends Rangers (Sh 200,000),
Lipuli (Sh 200,000), Majimaji (Sh 400,000),
Polisi Morogoro (Sh 400,000) na Transit Camp
(Sh 200,000).
Kocha Msaidizi wa Polisi Morogoro, John
Tamba atapelekwa kwenye Kamati ya Maadili
kutokana na vitendo visivyo vya kimaadili
katika mechi dhidi ya Burkina Faso.
Kiongozi wa Lipuli, Hamis Kiemba na
wachezaji Boniface Sawaka, George Enock na
Green Paul watapelekwa katika Kamati ya
Nidhamu kutokana na utovu wa nidhamu
waliofanya kwenye mechi dhidi ya Kimondo.
Naye mchezaji Sangalau Nyamoka wa JKT
Kanembwa aliyelalamikiwa uhalali wake na
Polisi Tabora, suala lake linapelekwa Kamati
ya Nidhamu.
Saturday, March 8, 2014
USHIRIKINA NA MATUSI VIMEWAPONZA SIMBA
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment