Monday, March 31, 2014

Shinyanga kurudi katika ligi kuu msimu ujao

HATIMAYE wapenzi wa soka wa Mkoa wa
Shinyanga watashuhudia tena mechi za Ligi
Kuu ya soka ya Tanzania Bara msimu ujao
tangu Kahama United ambayo hapo awali
ilikuwa ikiitwa Shinyanga United, iliposhuka
daraja mwaka 2006 na hivyo kubaki wakiisikia
michuano hiyo kwenye vyombo vya habari.
Hali hiyo inatokana na matokeo ya michezo
miwili ya Ligi Daraja la Kwanza Tanzania Bara
Kundi C mwishoni mwa wiki yaliyotoa
mwelekeo wa timu mbili za Shinyanga za
Mwadui FC na Stand United kushinda michezo
yao na kufikisha pointi ambazo haziwezi
kufikiwa na timu nyingine za kundi hilo.
Mwadui FC ikicheza kwenye uwanja wake wa
nyumbani, iliichapa Toto African ya Mwanza
kwa bao 1-0, lililofungwa na Ibrahim Hajib
katika dakika ya 11 na bao hilo kudumu hadi
mwisho wa mchezo huo na hivyo kujikita
kileleni mwa msimamo wa ligi hiyo kwa
kujikusanyia pointi 28 kwa michezo 13.
Stand United inashika nafasi ya pili katika
msimamo wa kundi hilo baada ya kuwaadhiri
wenyeji wao, JKT Kanembwa ya Kigoma
kwenye Uwanja wa Lake Tanganyika mjini
Kigoma kwa mabao 3-2 katika mchezo
uliokuwa wa funga nikufunge na hivyo Stand
United kufikisha pointi 26.
Kwa matokeo hayo, sasa vita ya kuwania
kutinga Ligi Kuu msimu ujao imebaki kwa timu
hizo mbili za Shinyanga baada ya timu hizo
kuwa na alama ambazo haziwezi kufikiwa na
timu nyingine huku zikiwa zimebakiwa na
mchezo mmoja kila moja.
Timu ambazo zilikuwa zinazikaribia timu hizo
za JKT Kanembwa imebakiwa na pointi 20 kwa
michezo 13 nayo ikiwa imebakiwa na mchezo
mmoja, lakini hata ikishinda itafikisha pointi 23
na Toto African yenye pointi 21 imebakiwa na
mchezo mmoja ambao ikishinda itafikisha
pointi 24.
Timu nyingine zilizoshiriki kwenye Kundi C
ambazo tayari zimepoteza matumaini ya
kucheza Ligi Kuu ni mabingwa wa zamani wa
Tanzania, Pamba, Polisi ya Tabora, Polisi ya
Mara na Polisi Dodoma.

No comments:

Post a Comment