Saturday, March 8, 2014

SIMBA NDANI YA MBEYA KUIKABIRI PRISONS

TIMU ya Simba iliwasili jana mkoani Mbeya
tayari kwa mchezo wao dhidi ya Tanzania
Prisons utakaochezwa kesho kwenye Uwanja
wa Sokoine jijini humo.
Simba ambayo kwa sasa ina pointi 35, iliwasili
mkoani humo ikiwa na mshambuliaji wake
nyota, Amisi Tambwe aliyejiunga na kikosi
hicho majuzi akitokea Kigali alipoenda
kuungana na timu yake ya Taifa, Burundi
iliyocheza mchezo wa kirafiki wa kimataifa
Jumatano iliyopita dhidi timu ya Rwanda.
Akizungumza na gazeti hili jana, Msemaji wa
Simba, Asha Muhaji alisema kujiunga kwa
mchezaji huyo kwenye kikosi hicho imeongeza
hamasa ya ushindi.
“Kama wachezaji na viongozi tumefurahishwa
na kurejea kwa mchezaji wetu huyu ambaye
aliruhusiwa kwenda kuchezea timu yake, na
kwa sasa kujiunga nasi tena ni furaha na
ishara ya ushindi,” alisema Muhaji.
Akizungumzia wachezaji wengine walioko
Taifa Stars na walikuwa kwenye msafara mjini
Windhoek, wakicheza mchezo wa kirafiki na
Namibia, Muhaji alisema mpaka jana jioni
walikuwa hawajawasili.
Alisema waliambiwa kuwa wangewasili juzi na
wakasubiri, lakini hadi anawasiliana na gazeti
hili walikuwa hawajawasili. Stars ilitarajiwa
kuwasili Dar es Salaam jana saa 12.45 jioni.
Alisema uliandaliwa utaratibu wa kuwapeleka
mkoani Mbeya na kujiunga na timu hiyo. Simba
ipo katika nafasi ya nne ikiwa na pointi 35,
nyuma ya Azam FC yenye pointi 40, Yanga
pointi 38 na Mbeya City yenye pointi 36.
Ligi Kuu itaendelea leo kwa mechi tatu ambapo
Coastal Union itaumana na Ashanti United
kwenye Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga.
Ruvu Shooting itaikaribisha Oljoro JKT kwenye
Uwanja wa Mabatini, Mlandizi mkoani Pwania
wakati Mbeya City itacheza na Rhino Rangers
kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine
jijini Mbeya.
Mechi za kesho ni Tanzania Prisons na Simba
kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine
jijini Mbeya, na JKT Ruvu na Mtibwa Sugar
zitacheza Uwanja wa Azam Complex uliopo
Chamazi, Dar es Salaam.

No comments:

Post a Comment