Saturday, March 8, 2014

MBIVU NA MBICHI KUJULIKANA LEO KULE JESHINI ALEXANDRIA...MUNGU IBARIKI YANGA...MUNGU IBARIKI TANZANIA

YANGA leo wanatupa karata yao muhimu
katika mchezo wa marudiano dhidi ya
mabingwa wa soka Afrika, National Al Ahly,
mchezo wa raundi ya kwanza wa Ligi ya
Mabingwa uliopangwa kufanyika kwenye
Uwanja wa Berg El Arab mjini Alexandria nchini
Misri.
Mchezo huo unatarajia kuanza saa 1 kamili
kwa saa za Misri, sawa na saa 2 usiku za
Tanzania na Yanga itaingia uwanjani ikiwa
mbele kwa bao 1-0 ililolipata kwenye Uwanja
wa Taifa, Dar es Salaam wiki iliyopita.
Ushindi wa Yanga ulionekana kuwakera Al Ahly
ambao waliondoka na mipango kadha wa
kadha ili kuhakikisha wanapata ushindi katika
mchezo wa leo ambao utawasaidia kusonga
mbele ili wautetee ubingwa wao ambao
wanaumiliki hadi sasa.
Kuchanganyikiwa kwa Al Ahly pengine ni
kutokana na kiwango cha Yanga
kuwashangaza mabingwa hao watetezi, kiasi
kwamba walishindwa kutangaza mapema
uwanja utakaotumika leo kabla ya Chama cha
Soka Misri kuingilia kati na kuamuru pambano
hilo lipigwe kwenye dimba la Berg El Arab,
Alexandria.
Kwa upande wao, Yanga wanaonekana kupania
kushinda baada ya kuwahi kwenda Misri
mapema tangu alfajiri ya Alhamisi walikuwa
Cairo, na katika kuonekana wamepania,
walikataa huduma zote ambazo waliandaliwa
na wenyeji wao, ikiwemo basi la kuwabeba
kutoka uwanja wa ndege kwenda hoteli na pia
waliamua kujipangia hoteli yao na siyo ile
ambayo waliandaliwa na Al Ahly.
Mikakati ya viongozi wa Yanga kuepuka
hujuma za Al Ahly iliendelea baada ya
kugomea usafiri wa ndege kutoka Cairo
kwenda Alexandria, na kuamua kwenda kwa
usafiri wa basi waliloandaliwa na Ubalozi wa
Tanzania nchini humo.
Ingawa Kocha Mkuu wa Yanga, Hans van de
Pluijm alisema kikosi chake kipo tayari kwa
mchezo na hawatacheza kwa kupaki basi,
badala yake watashambulia kama
walivyofanya nyumbani, njia hiyo ni nzuri
kwao, lakini anapaswa kuwakumbusha
wachezaji wake wacheze kwa umakini
mkubwa na kuwakumbusha kila wakati kurudi
nyuma kwa ajili kuwasaidia mabeki wao
kuzuia mashambulizi.
Ni wazi Al Ahly wataingia mchezoni kwa kasi
kubwa wakihitaji kupata mabao ya mapema ili
kujiwekea matumaini ya kusonga mbele, hivyo
Yanga wanatakiwa kucheza kwa tahadhari
hasa sehemu ya ulinzi ambayo itatakiwa kuwa
makini kwa kuwachunga washambuliaji hatari,
Mohamed Ismail ‘Mido’ na Amri Gamal ambao
ndiyo tegemezi katika ufungaji.
Wanachotakiwa kukifanya Yanga ni kutulia na
kucheza mpira wao kama walioucheza kwenye
mechi ya kwanza na ikiwezekana zaidi ya huo,
na wapate bao moja la mapema ambalo
litawachanganya Al Ahly ambao watakuwa
wakicheza pasipo mashabiki, kitu ambacho
kitawarahisishia kazi wawakilishi hao wa
Tanzania na kujikuta wakiwavua ubingwa
mabingwa hao wa Afrika.
Endapo Yanga itafanikiwa kuwabana Al Ahly
kwa dakika 30 pasipokuruhusu bao, kuna
uwezekano mkubwa timu hiyo ikafanikiwa
katika harakati zake zote ilizozifanya na
kuwatoa Al Ahly ambayo kabla ya mchezo wa
leo, mambo yao kwenye uongozi si shwari na
hata mwenendo kwenye ligi ya Misri siyo
mzuri.

No comments:

Post a Comment