Saturday, March 29, 2014

Tathmini mechi za leo ligi kuu bara

MBIO za kuwania ubingwa wa Ligi Kuu
Tanzania Bara zinaendelea leo kwa timu tatu
zenye nafasi ya kutwaa taji hilo kushuka
kwenye viwanja vitatu tofauti kuwania pointi
tatu muhimu.
Mchezo wa kwanza utawakutanisha vinara wa
ligi hiyo Azam FC,ambao watakuwa uwanja wa
Taifa Dar es Salaam kupambana na Simba
mchezo ambao umevuta hisia za mashabiki
wengi wanaotaka kujua kama Simba
itakwamisha ndoto za Azam kutwaa ubingwa
msimu huu.
Mchezo huo unatarajiwa kuwa mgumu kwa
pande zote mbili hasa kwa Azam ambayo
itataka kushinda ili kuikimbia Yanga
inayoifukuzia kwa kasi kileleni licha ya tofauti
ya pointi nne zilizopo kati yao. Azam ina pointi
50 na Yanga 46.
Azam itaingia kwenye mchezo huo wa leo
ikiwa na kumbukumbu nzuri ya ushindi wa
mabao 2-0 iliyoupata Jumatano iliyopita dhidi
ya Mgambo JKT,kwenye uwanja wa
Mkwakwani jijini Tanga.
Ni wazi kwamba itahakikisha inatumia kila aina
ya mbinu ili kupata ushindi katika mchezo huo
muhimu kwao kwa sababu inajua fika endapo
itateleza na kupoteza au kutoka sare itakuwa
imewapa nafasi nzuri wapinzani wao Yanga
kuwa na matumaini makubwa ya kutetea
ubingwa wao.
Lakini ugumu wa mchezo huo unakuja pale
ambapo Simba ambayo licha ya kuwa haina
cha kupoteza katika mchezo huo lakini
haitakubali kufungwa mara ya pili mfululizo na
Azam, kwani katika mechi ya raundi ya kwanza
ililala kwa mabao 2-1.
Kocha wa Simba, Zdravko Logarusic amesema
atahakikisha leo anapanga kikosi imara
ambacho kitambana na kupata ushindi wa
pointi zote tatu ili angalau kuwapoza machungu
mashabiki wao ambao wana kumbukumbu
mbaya ya timu yao kufungwa bao 1-0 na
Coastal Union wiki iliyopita.
Kivumbi kingine kitakuwa kwenye Uwanja wa
Mkwakwani Tanga wakati mabingwa watetezi
Yanga watakapokuwa wakikabiliana na
Maafande wa Mgambo JKT.
Yanga inaingia kwenye mchezo huo ikiwa na
kumbukumbu nzuri ya ushindi mnono wa
mabao 5-0 ilioupata Jumatano iliyopita dhidi ya
Prisons na ni wazi itacheza kwa juhudi ili
kushinda mchezo huo ili kuzidi kuifukuzia
Azam iliyopo kileleni.
Kocha wa Yanga Hans Van Der Plyuijm,
amesema kila mchezo kwao ni fainali na
hawataidharau timu yoyote lengo lao likiwa
kushinda mechi zote saba zilizobaki ili kutetea
ubingwa wao.
Van Der Plyuijm alisema vijana wake
wameonesha ari kubwa ya kujituma na kupata
ushindi katika mechi tatu zilizopita hivyo hana
shaka hata katika mchezo wa leo watafanya
hivyo ili kuendelea kufukuzia ubingwa huo kwa
mara ya 25.
Mgambo JKT, ambayo haipewi nafasi ya
kushinda katika mchezo wa leo itaingia na
hasira kubwa ya kutaka kuiaibisha Yanga
baada ya kupoteza mchezo wake uliopita na
Azam FC.
Ukiacha hasira za kupoteza mchezo uliopita
kitu kingine kitakachoifanya Mgambo
kutokubali kupoteza mchezo huo ni nafasi ya
11 iliyopo kwenye msimamo ambayo ni mbaya
na huenda ikashuka daraja kama itaendelea
kupoteza mechi zake.
Mgambo ina pointi 19, na imesaliwa na
michezo mitano ili kumaliza msimu hivyo
itataka kushinda kama ilivyofanya kwa Simba
Februari 9 na kujiweka katika mazingira
mazuri ya kunusurika kushuka daraja.
Mtanange mwingine ambao leo utakuwa
unahusishwa na mbio za ubingwa ni ule
utakaowakutanisha ndugu wawili Mbeya City
na Prisons ambazo zitapambana kwenye
uwanja wa Sokoine Mbeya.
Timu hizo zitaingia katika mchezo huo zikiwa
katika hali tofauti katika mechi zao zilizopita,
Mbeya City wakitoka kuibuka na ushindi wa
mabao 2-0 ugenini dhidi ya JKT Ruvu wakati
Prisons ikikiona cha mtemakuni baada ya
kufungwa 5-0 na Yanga.
Mbeya City iliyopo kwenye kiwango bora kwa
sasa inapewa nafasi ya kushinda mchezo huo
lakini wapinzani wao Prisons siyo timu ya
kubeza licha ya kipigo hicho walichokipata
kutoka kwa Yanga.
Prisons imeonekana kuimarika zaidi kwenye
mzunguko wa pili ikiwemo kutoa vipigo kwa
timu ngumu kama Mtibwa Sugar iliyokuwa
kwenye uwanja wao wa nyumbani na kipigo
cha 6-0, ilichoipa JKT Ruvu.
Pamoja na Mbeya City kujipa matumaini ya
kushinda mchezo huo lakini isitarajie
mteremko kwani Prisons ya sasa siyo ile ya
mzunguko wa kwanza ambayo ilipata pointi 9
kwenye mechi 13 ilizocheza duru la kwanza.

No comments:

Post a Comment