Monday, March 24, 2014

Ronaldo: Marefa wanatuonea

Mchezaji bora duniani, Cristiano Ronaldo amesema
kwamba marefa hawawatendei haki kila
wanapokutana na wapinzani wao wa jadi,
Barcelona.
Ametoa kauli hiyo baada ya Real Madrid kufungwa
4-3 na mabingwa hao wa Hispania kwenye mechi
ya kukata na shoka Jumapili hii.
Ronaldo anasema kwamba haielezeki jinsi maamuzi
mabaya yanavyotolewa na waamuzi kwenye mechi
baina yao, ambapo Jumapili hii Real Madrid
walikuwa wamejiamini sana kwamba wangeshinda
kutokana na rekodi yao ya hivi karibuni.
Katika mechi hiyo, mwamuzi Alberto Undiano
Mallenco alitoa penati tatu lakini pia alimyoa nje kwa
kadi nyekundu mchezaji Sergio Ramos wa Real
Madrid katika uwanja wao wa nyumbani wa
Santiago Bernabeu.
Lionel Messi alitupia mabao mawili kwa penati tata
kama sehemu ya hat-trick yake, ambapo Barca
walitoka kusinzia 3-2 na kuwalaza Madrid 4-3 na
kufufua upya ndoto zao za ubingwa.
“Ni ngumu sana kwa sababu watu wengi
hawakutaka tushinde kwa vile kwa kufanya hivyo
Barcelona wangekuwa wametupwa nje ya
kinyang’anyiro cha ubingwa wa Hispania. Labda
hawataki tuchukue kombe hili,” alisema Ronaldo.
Mreno huyo mwenyewe alifunga bao kwa penati tata
pia baada ya Dani Alves kumwangusha nje ya boksi
la penati. Ramos alipotolewa nje kwa kumpiga
kwanja Neymar kwenye mstari wa boksi, wageni
waliona kwamba wakati wao wa kujidai ulifika, na
kweli Messi akasawazisha kwa penati.
Barca ndio walikuwa wa kwanza kupata bao katika
dakika ya saba kupitia kwa Andres Iniesta lakini
likasawazishwa na Karim Benzema dakika ya 24
kabla Mfaransa huyo huyo hajaongeza jingine
dakika ya 24.
Hata hivyo, penati aliyotumbukiza kwenye kwamba
Messi ilikuja dakika ya 42 kabla ya hasimu wake,
Ronaldo kufunga yake dakika ya 55. Dakika 10
baadaye Messi alifunga tena kwa penati dakika ya
65 kabla ya kufumania nyavu dakika sita kabla ya
mechi kumalizika.
“Tunasikitika sana kwa matokeo haya, kwa sababu
ukweli ni kwamba tulitakiwa tushinde sisi,”
akasema Ronaldo ambaye wakati wa mechi alifika
mahali akamfuata mwamuzi kumlalamikia.
Matokeo hayo yanawafanya Atletico Madrid
kuongoza ligi kwa kufikisha pointi 70 sawa na Real,
huku wakifuatiwa na Barca wenye pointi moja
pungufu na Athletic Bilbao wenye pointi 55.

No comments:

Post a Comment