Monday, March 24, 2014

Mkwasa akiri mechi dhidi ya prisons itakua ngumu

MABINGWA watetezi wa Ligi Kuu ya soka
Bara, Yanga wamesema pambano dhidi ya
Tanzania Prisons sio mechi rahisi kama
ambavyo wengi hudhani, hivyo wana kazi ya
kujipanga ili kuchukua pointi tatu muhimu.
Yanga wamerejea Dar es Salaam juzi
wakitokea Tabora walikokuwa na mechi dhidi
ya Rhino Rangers ambako walipata ushindi wa
mabao 3-0 katika mchezo uliofanyika kwenye
Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi na jana jioni
ilitarajiwa kuanza kujifua kwenye uwanja wake
tayari kwa mechi ya kesho.
Mabingwa hao wa Bara wanatarajiwa kushuka
dimbani kesho kuvaana na maafande hao wa
Magereza kutoka Mbeya katika mechi
itakayochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar
es Salaam.
Akizungumza na gazeti hili jana, Kocha
Msaidizi wa Yanga, Charles Boniface Mkwasa
alisema katika kuelekea mwishoni mwa
msimu, kila timu hujipanga kufanya vizuri ili
kuendelea kubaki katika nafasi nzuri, hivyo
anafikiri mechi hiyo huenda ikawa ngumu.
“Tunaelekea mwishoni mwa msimu, upinzani
utakuwa ni mkali kwa sababu kila timu
inajipanga kubaki katika nafasi nzuri, na wakati
huo, tusipokuwa makini mchezo utakuwa ni
mgumu,” alisema Mkwasa ambaye alifundisha
na kuipa ubingwa wa Tanzania, Prisons
mwaka 2000.
Mkwasa alisema wachezaji wake wote wako
salama hivyo wataendelea na mazoezi mepesi
jana na leo tayari kwa mchuano huo wakiwa na
lengo la kufanya vizuri ili kuchukua tena
ubingwa.
Kuhusu kipa wao namba moja, Deogratius
Munishi, Mkwasa alisema hajapata uhakika
kama atakuwepo mpaka apate maelezo ya
daktari wao.
Kwa upande wake, daktari wa Yanga, Juma
Sufiani alisema Munishi anaendelea na
matibabu na hajawasiliana naye kuona kama
amepata nafuu kwa vile alikuwa safarini.
Katika msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara,
Yanga iko katika nafasi ya pili ikiwa na pointi
43 nyuma ya Azam yenye pointi 47, wakati
Tanzania Prisons iko katika nafasi ya 10 ikiwa
na pointi 22.
Hata hivyo, Yanga iko nyuma mchezo mmoja
na Azam FC kesho itakuwa Tanga kuikabili
Mgambo JKT.

No comments:

Post a Comment