MBEYA City jana ilikwea hadi nafasi ya pili
katika msimamo wa Ligi Kuu ya soka ya
Tanzania Bara baada ya kuifunga Rhino
Rangers ya Tabora kwa mabao 3-1. Katika
mechi hiyo iliyochezwa kwenye Uwanja wa
Kumbukumbu ya Sokoine jijini hapa, mabao ya
washindi yalifungwa na Saad Kipanga mabao
mawili na Deus Kaseke. Bao la Rhino lilifungwa
na Yohana Morris wa Mbeya City aliyejifunga
mwenyewe.
Kwa matokeo hayo, kikosi cha Juma
Mwambusi, kimeishusha Yanga katika nafasi
ya pili kwa kufikisha pointi 39 wakati Yanga
inashuka nafasi ya tatu ikiwa na pointi 38.
Azam FC iko kileleni kwa pointi 40. Rhino
Rangers ilikuwa ya kwanza kupata bao katika
dakika ya pili, ambalo Morris alijifunga wakati
akimrudishia mpira kipa wake, David Burhan,
kutokana na shambulizi la timu hiyo ya Tabora.
Iliwachukua dakika sita tu wenyeji
kusawazisha kwa bao la Kipanga kutokana na
shuti kali baada ya kupokea krosi ya Kaseke.
Kipanga aliongeza bao jingine kwa shuti kali
lililotinga katika nyavu ndogo kutokana na pasi
maridadi ya Kaseke tena. Mbeya City
walijihakikisha pointi tatu muhimu baada ya
Kaseke kufunga bao katika dakika ya 34,
kutokana na mpira alioupiga kwenda moja kwa
moja wavuni na kumuacha kipa wa Rhino
Rangers, Charles Mpinuki, akiwa hana la
kufanya.
Kaseke alipokea mpira wa kona fupi uliopigwa
na Hassan Mwasapili. Rhino Rangers
inakamata mkia ikiwa na pointi 13 baada ya
kucheza mechi 20.
Mjini Tanga, wenyeji Coastal Union walibanana
mbavu na Ashanti United ya Dar es Salaam na
kwenda sare ya kutofungana, hivyo Wagosi wa
Kaya kufikisha pointi 26, wakati Ashanti sasa
ina pointi 15.
Kwenye Uwanja wa Mabatini, Mlandizi mkoani
Pwani, wenyeji Ruvu Shooting waliishinda JKT
Oljoro ya Arusha kwa bao 1-0, lililofungwa na
Ayoub Kitala.
Kwa matokeo hayo, Ruvu Shooting imefikisha
pointi 28 na imefika nafasi ya sita, nyuma ya
Kagera Sugar yenye pointi 29, wakati JKT
Oljoro imebaki na pointi zake 15 na imecheza
mechi 21.
Ligi hiyo inaendelea leo kwa mechi mbili kati
ya Tanzania Prisons dhidi ya Simba kwenye
Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine jijini
Mbeya na JKT Ruvu itaikaribisha Mtibwa Sugar
kwenye Uwanja wa Azam Complex, nje kidogo
ya Jiji la Dar es Salaam.
Kundi la kwanza la Simba liliwasili jijini Mbeya
juzi wakati kundi lingine wakiwamo wachezaji
waliokuwa katika timu ya Taifa iliyocheza
Namibia Jumatano wiki hii, waliwasili humo
jana. Ushindi kwa Simba leo utaifikisha katika
pointi 38, sawa na Yanga ambayo hata iko
nyuma kwa michezo minne kutokana na
ushiriki wao katika michuano ya kimataifa.
Kwa upande wake, Prisons imezinduka katika
msimamo wa Ligi Kuu na imecheza mechi 17,
ikiwa nafasi ya 10 kwa kuwa na pointi 17.
Chini ya kocha David Mwamwaja, timu hiyo
inaonekana kuwa mwiba na leo inatarajiwa
kuwa itaichezesha mchakamchaka Simba.
JKT Ruvu na Mtibwa Sugar zote ziko katikati
ya msimamo, ingawa mwenendo wa zote mbili
unaonekana kutokuwa mzuri katika mzunguko
wa pili unaotarajiwa kufikia tamati Aprili 27,
mwaka huu.
Saturday, March 8, 2014
MBEYA CITY MWENDO MDUNDO
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment