Wednesday, March 26, 2014

Kipa wa KMKM afariki dunia

KLABU ya soka ya KMKM ya Zanzibar imepata
pigo kubwa la kuondokewa na kipa wake, Ali
Suleiman Bishoo, aliyefariki usiku wa kuamkia
jana.
Bishoo aliyekuwa kipa namba moja, alifariki
kwa kuangukiwa na mti wa aina ya mvinje
kutokana na upepo mkali uliovuma. Alifariki
dunia saa nane usiku baada ya kukutwa na
ajali akiwa na Vespa katika maeneo ya
Mwanakwerekwe Wilaya ya Magharibi Unguja.
Kwa mujibu wa Katibu wa timu hiyo, Sheha
Mohammed, kipa huyo alikutwa na mauti
wakati akitoka katika safari zake za kawaida.
“Tumepata pigo kubwa, lakini kazi ya Mungu
haina makosa…sisi tulimpenda, lakini yeye
amempenda zaidi,” alisema Katibu huyo.
Mwili wa marehemu ulihifadhiwa katika
Hospitali ya Rufaa ya Mnazi Mmoja na
ulitarajiwa kuzikwa jana kijijini kwao Cheju
Mkoa wa Kusini Unguja.
Bishoo alikuwa ni miongoni mwa makipa
waliochaguliwa katika timu ya Taifa ya
Zanzibar ‘Zanzibar Heroes’, lakini alizuiwa na
KMKM, hivyo kufungiwa kutocheza soka kwa
msimu mzima wa ligi na ZFA Taifa.
Awali, mabaharia hao wa KMKM juzi
walijiweka katika mazingira mazuri katika
msimamo wa Ligi Kuu ya Zanzibar baada ya
kufikisha pointi 36 kutokana na ushindi wa
mabao 2-0 dhidi ya Jamhuri.
Jamhuri katika mchezo huo watapaswa
kujilaumu kutokana na kukosa mabao mengi
ya wazi pamoja na penalti iliyopigwa na
Suleiman Ali Nuhu katika dakika ya 82.
Mabao ya KMKM yaliyowawezesha kuondoka
na ushindi huo yalifungwa na Mudriki Muhibu,
moja akilifunga katika dakika ya 14 na la pili
dakika ya 44.
KMKM sasa inashika nafasi ya pili, huku Polisi
ikiongoza kwa pointi 37, na kubakiwa na
michezo miwili, ambayo kama Polisi ikipoteza
mmoja na KMKM kushinda yote, basi
itatawazwa bingwa.

No comments:

Post a Comment