Monday, March 24, 2014

Singano(messi) akokotwa polisi

WINGA machachari wa Simba, Ramadhan
Singano juzi alilazimika kupelekwa kwenye
Kituo cha Polisi cha Chang’ombe katika Mkoa
wa Kipolisi wa Temeke, na Katibu Mkuu wa
timu hiyo, Ezekiel Kamwaga.
Hiyo ilitokana na mchezaji huyo kuvunja kioo
cha moja ya mlango wa kuelekea kwenye
vyumba vya kubadilishia nguo uwanjani hapo
kwa kukipiga teke, muda mfupi baada ya
mchezo kati yao na Coastal Union ya Tanga
kumalizika wakiwa wamelala kwa bao 1-0.
Kutokana na kitendo hicho cha utovu wa
nidhamu na uharibifu wa mali ya umma, askari
Polisi waliokuwepo uwanjani wakilinda
usalama, walipanga kuondoka na mchezaji
kumpeleka kituoni, lakini viongozi wa timu hiyo
waliingilia kati na kuamua kumpeleka wao ili
akatoe maelezo.
“Katibu wetu Kamwaga (Ezekiel) ndiye
aliyempeleka Singano, kituo cha Polisi ili
akaandike maelezo kuhusu uharibifu
alioufanya. Ni kweli askari wa Jeshi la Polisi
walipanga kuondoka naye, lakini tulizungumza
nao hasa kwa kuzingatia jina alilokuwa nalo
mchezaji,” alisema Mjumbe wa Kamati ya
Utendaji ya Simba, Saidi Pamba.
Pamba alisema baada ya kuandikisha maelezo,
mchezaji huyo ambaye pia anaichezea Taifa
Stars, aliachiwa huru huku wakisubiri Jeshi
hilo lifanye kazi yake kwa kushirikiana na
mamlaka husika kwa maana ya Shirikisho la
Soka (TFF) na Uwanja wa Taifa kufahamu
gharama ya uharibifu alioufanya winga huyo.
“Tunasubiri ripoti ya Polisi iweze kutoa majibu
baada ya kumaliza uchunguzi endapo
atatakiwa kulipa faini hiyo, atalazimika
kulimaliza mchezaji mwenyewe na kama
atakuwa hana Simba itamlipia, lakini kwa
masharti ya kumkata kwenye mshahara
wake,” alisema Pamba.
Katika mchezo huo, Singano alipoteza nafasi
nyingi za kufunga mabao ikiwemo ile ya dakika
ya mwisho aliyoipata na kushindwa kuisaidia
timu yake kuepuka na kipigo katika mchezo
huo.
Kutokana na matokeo hayo yaliyowakera
mashabiki wa timu hiyo, Pamba alisema jana
Kamati ya Utendaji pamoja na ile ya Ufundi
zilitarajiwa kuwa na mkutano kujadili sababu
ya timu hiyo kufanya vibaya na namna gani ya
kushinda mechi nne zilizosalia kabla msimu
huu haujamalizika.
Katika msimamo wa ligi, Simba inashika nafasi
ya tatu ikiwa na pointi 36, pointi sita nyuma ya
wanaoshika nafasi ya tatu Mbeya City, pointi
saba nyuma ya Yanga na pointi 11 nyuma ya
vinara.

No comments:

Post a Comment