KAMA ilivyokuwa kwa Chelsea katika Ligi Kuu
ya England juzi kwa kufungwa na kutibuliwa
mbio za kuwania taji la nchi hiyo, Yanga jana
ilipata pigo kama hilo kutoka kwa Mgambo JKT
ya Tanga.
Wakati Chelsea ikilala kwa bao 1-0 kutoka kwa
Crystal Palace na kocha wake mbwatukaji,
Jose Mourinho akikiri mbio za ubingwa
zimekwisha, mabingwa watetezi wa Bara,
Yanga jana walichapwa mabao 2-1 na timu
hiyo ya Kabuku wilayani Handeni na kuwapa
pigo kubwa katika mbio za ubingwa.
Kwa matokeo hayo, Yanga imebakiwa na pointi
46 katika nafasi ya pili huku timu waliyokuwa
wakibanana nayo, Azam FC imefikisha pointi
53 baada ya jana kuishinda Simba kwenye
Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Yanga sasa imebakiwa na mechi nne dhidi ya
JKT Ruvu, Kagera Sugar, JKT Oljoro na Simba,
ambazo kama ikishinda zote, itafikisha 58
wakati Azam FC imebakiza mechi tatu dhidi ya
Ruvu Shooting, Mbeya City na JKT Ruvu
ambazo ikishinda zote, itafikisha pointi 62 na
kutawazwa bingwa msimu wa 2013/14.
Kwa Yanga, matokeo ya jana kwenye Uwanja
wa Mkwakwani jijini Tanga, ni pigo kubwa
kwao kwani sasa inabidi waiombee dua mbaya
Azam FC na yenyewe ikihitaji kushinda mechi
zilizobaki ili itetee ubingwa.
Mgambo JKT ilikuwa ya kwanza kuandika bao
katika dakika ya pili tu lililofungwa na Fully
Maganga, ambalo lilidumu hadi mapumziko.
Iliwachukua Yanga dakika nane za kipindi cha
pili kusawazisha kwa penalti iliyokwamishwa
wavuni na nahodha Nadir Haroub.
Bao lililoipa pigo Yanga lilifungwa kwa penalti
katika dakika ya 65 baada ya mwamuzi Alex
Mahagi wa Mwanza kuamuru pigo hilo la
adhabu kubwa kutokana na beki Kelvin
Yondani kumfanyia madhambi Malimi Busungu
akielekea kufunga.
Busungu alipiga penalti hiyo na kumfunga kipa
Juma Kaseja, na kuandika bao la pili ambalo
licha ya juhudi kubwa za Yanga kutaka
kusawazisha, hali haikuwa rahisi na hivyo
Mgambo JKT kuandika ushindi wake wa pili
mkubwa msimu huu, kwani kwenye uwanja
huo, waliifunga Simba kwa bao 1-0.
Sunday, March 30, 2014
Yanga hoiiiiii ,Tanga
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment