WADHAMINI wa Yanga wametoa maelekezo
kwa mawakili wao kuweka pingamizi katika
Mahakama ya Kazi kuzuia mali zao kushikiliwa
na Shirikisho la Soka Tanzania(TFF) bila wao
kuhusishwa katika mchakato.
Hivi karibuni TFF ilisema imepokea amri ya
Mahakama Kuu (Kitengo cha Kazi) kukamata
Sh milioni 106 za Yanga kutokana na mapato
ya mlangoni kwenye mechi zake ili kuwalipa
waliokuwa wachezaji wake Stephen Malashi
na Wisdom Ndlovu, agizo ambalo TFF
imeshaanza kulitekeleza.
Wachezaji hao waliingia mkataba na Yanga
mwaka 2010, lakini Yanga ilivunja mikataba
yao na hivyo kuamua kufungua kesi
mahakamani kupinga suala hilo na kutaka
walipwe haki zao ambapo mahakama
ikaamuru walipwe Sh milioni 106.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotumwa kwa vyombo
vya habari jana na kusainiwa na Katibu Mkuu
wa Yanga, Beno Njovu, sheria ya usajili wa
wadhamini Cap. 318 na kanuni za kesi za
madai zote zinatakiwa kuwa kama mali zozote
zilizo chini ya wadhamini hivyo wanatakiwa
kuuhusishwa katika mchakato wa kesi hiyo.
“Wafaidika hawawezi kwa mujibu wa sheria
kushtakiwa mahakamani wakati wao ni
wafaidika tu wa mali zilizo chini ya udhamini,”
ilisema taarifa hiyo.
Pia, ilisema wadhamini hao wamewapa
maelekezo mawakili kufanya maombi
yanayohitajika kwa Majaji wa Mahakama ya
Kazi kuomba marejeo ya mwenendo wa kesi
na namna gani sheria iliweza kupindishwa
katika Baraza la Usuluhishi na Uamuzi na
kuona hatua gani za kurekebisha hali hiyo
zinaweza kuchukuliwa.
Taarifa hiyo ilisema wachezaji wote wawili ni
watu wasio na makazi ya kudumu na kwamba
mmojawao ameshawahi kulipwa kupitia TFF na
haijawahi kutiliwa maanani na kuongeza:
“Yanga inaamini Jaji wa Mahakama Kuu
akiongozwa vizuri atatoa nafuu stahiki”.
Taarifa hiyo ilisema, wameamua kupeleka
malalamiko yao kwa Jaji Mkuu wa Tanzania ili
kuona kama utaratibu wa kiutawala ulifuatwa
na kutekelezwa kwa usahihi pamoja na
kutokuwepo kwa faili la Mahakama ambalo
lilikuwa tayari katika Mahakama ya Rufaa
kutokana na kuwepo kwa maombi mawili
namba 163 ya mwaka 2013 na 165 ya mwaka
huo.
Ilisema wakati maombi namba 163 yalifutwa
mwaka huo, mengine hayajaitwa kwa ajili ya
kusikilizwa au kufutwa. Taarifa hiyo ilifafanua,
wadhamini ndio wamiliki wa mali zote za
Yanga bila kujali kuwa zisizohamishika,
zinazohamishika au fedha hivyo kuhoji ni kwa
namna gani TFF inaruhusu utekelezaji wa amri
dhidi ya klabu na si wadhamini.
“Sisi tunathubutu kusema kwamba TFF
ilipaswa kuijibu Amri ya Mahakama kwamba
wao hawana fedha ya klabu ambao ni
wafaidika,” alisema. “Hatua ya kuruhusu fedha
za wadhamini kushikiliwa ni kinyume cha
sheria hivyo tunaitaka irudishe fedha hizo
pamoja na riba yake au itufikishe mbele ya
vyombo vya sheria kwa matumizi mabaya ya
fedha za wadhamini."
Wednesday, April 2, 2014
Yanga kuipeleka TFF kizimbani
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment