RAIS Jakaya Kikwete amesema klabu ya Azam
FC inajitahidi katika uwekezaji wa soka kwa
vijana na kuitabiria kufika mbali katika soka
Afrika.
Kauli yake imekuja siku chache baada ya klabu
hiyo ya Chamazi nje kidogo ya Jiji la Dar es
Salaam, kutwaa ubingwa wa Tanzania Bara
kwa mara ya kwanza tangu ianzishwe mwaka
2007.
Rais Kikwete alisema hayo Ikulu, Dar es
Salaam juzi katika mahojiano maalumu na
kituo cha televisheni cha TBC1, mali ya Shirika
la Utangazaji Tanzania (TBC), yaliyohudhuriwa
pia na waandishi wa habari wa vyombo vingine
kuhusu miaka 50 ya Muungano.
Alisema hayo alipojibu swali la mwandishi
aliyetaka kujua maoni yake kuhusu maendeleo
ya michezo nchini.
“Tatizo letu ni menejimenti ya soka katika
klabu zetu. Mfano, Yanga na Simba
wangewekeza katika timu za watoto wa umri
mbalimbali na kuwa na utulivu, zingepiga hatua
kubwa,” alisema Rais Kikwete.
Alisema klabu inayojitahidi kuwekeza katika
soka nchini ni Azam, ambayo imewekeza kwa
vijana.
“Naamini Azam itakuwa timu kubwa Afrika kwa
sababu wana A,B,C za kuendeleza michezo,”
alisema.
Amesema klabu za Yanga na Simba, haziishiwi
na migogoro na migogoro hiyo imezorotesha
maendeleo ya soka nchini. Alisema timu hizo
maarufu nchini, zimekuwa zikipokezana
migogoro, yaani ukiisha Yanga, unahamia
Simba.
Rais Kikwete alisema Tanzania, watu
hawawekezi kwenye soka, bali wanawekeza
kwenye migogoro na mfano wa wanaowekeza
kwenye migogoro ni klabu za Yanga na Simba.
Rais Kikwete alisema kama Yanga na Simba,
zingekuwa na utulivu, zingewekeza kwa
wachezaji, ikiwemo kuendeleza timu za watoto
wa umri mbalimbali, hivyo kusonga mbele kwa
kasi. Mbali na soka, Rais alisema nchi
haijafanya vizuri katika riadha, netiboli, ngumi
na michezo mingine.
Alisema kila mara anapozungumzia suala la
michezo, suala hilo humpa uchungu. Alisema
tangu alipoingia madarakani, alijitahidi kusaidia
sekta hiyo, lakini bado haijawa na mafanikio.
Alisema katika hotuba yake ya mwaka 2005,
aliahidi mambo kadhaa, ikiwemo kuajiri kocha
wa timu ya taifa ya soka, na kweli alifanya
hivyo kwa kumuajiri Marcio Maximo.
“Niliwaambia kuwa miye nitaajiri kocha, nyie
mumhudumie kwa mahitaji mengine kama gari.
Nimefanya hivyo katika michezo mingine kama
netiboli, ngumi na riadha,” alifafanua Rais
Kikwete.
Alisema tatizo kubwa, lililopo katika sekta ya
michezo ni viongozi kushindwa kutimiza
mahitaji mengine ya makocha wa taifa, mfano
kuwapatia usafiri (magari).
Alilitaja tatizo jingine kubwa ni viongozi wa
michezo nchini, kushindwa kuwekeza kwenye
klabu zao, mfano kuwekeza kwa wachezaji.
Alisema timu za Ulaya zimepiga hatua kubwa,
kutokana na kuwekeza kwa wachezaji.
“Timu kubwa duniani kama Barcelona
zimewekeza kwa wachezaji hivyo na sisi
tuwekeze kwa wachezaji,” alisema rais.
Friday, April 18, 2014
J.K haipa tano Azam fc
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment