UONGOZI wa Yanga umesema hauna mpango
wa kuwatimua wachezaji wake wakati huu ligi
ikiwa inaendelea na zaidi inafikiria kwa vipi
itaimarisha kikosi chake kitetee ubingwa wa
Ligi Kuu Tanzania Bara.
Baada ya kumalizika kwa mechi kati ya Yanga
dhidi ya Mgambo JKT mwishoni mwa wiki
iliyopita, kumekuwa na uvumi wa kufukuzwa
kwa baadhi ya wachezaji waliovurunda katika
mchezo huo.
Katika mchezo huo, Yanga ilipata kipigo cha
mabao 2-1 katika mchezo uliofanyika kwenye
Uwanja wa CCM Mkwakwani, Tanga na hivyo
kutibua mbio zao za kutetea ubingwa na
kubaki katika nafasi ya pili ikiwa na pointi 46,
mashabiki wake wakiwa na hofu kutochukua
taji baada ya kukimbizwa kwa pointi na Azam.
Akizungumza na gazeti hili jana, Katibu Mkuu
wa Yanga, Beno Njovu alisema mpaka sasa
hakuna mchezaji aliyefukuzwa isipokuwa kuna
baadhi yao walienda kupumzika wakidai kuwa
wanaumwa.
“Inasikitisha sana kuona baadhi ya watu
wanasema tumewafukuza wachezaji, jambo
ambalo si la kweli, wachezaji wote bado tunao
na tutaendelea kuwatumia katika mechi
zilizobaki,” alisema Njovu.
Alisema ukweli ni kwamba Athumani Idd ‘Chuji’
alitoa taarifa kwa kocha wake kwamba
anaumwa tangu juzi hivyo alishindwa kushiriki
kwenye kambi ya Bagamoyo kwa ajili ya
maandalizi ya mechi ijayo dhidi ya JKT Ruvu
itakayochezwa kwenye Uwanja wa Taifa
keshokutwa.
Wachezaji wengine waliotoa taarifa ni Kelvin
Yondani ambaye alidai ana tatizo la kifamilia.
“Yondani alisema ana tatizo akaruhusiwa
kwenda kupumzika, nafikiri pengine ni kwa
sababu alikuwa ana kadi nyekundu hivyo hata
angeshiriki kwenye mazoezi, asingeweza
kucheza mechi ijayo,” alisema Njovu.
Kwa upande wa kiungo Haruna Niyonzima,
alisema bado anaumwa na tatizo lake
linajulikana kwa muda hivyo alipewa ruhusa
kabla
hata ya mechi ya wiki iliyopita.
Alisema wachezaji wengine wote wako
kambini wakiendelea na mazoezi ya kujifua
tayari kwa mechi ijayo ambayo kama nyingine
zilizobaki, ni muhimu kwa mabingwa hao
watetezi.
Tangu kufungwa na Mgambo JKT kwa mabao
hayo 2-1 ambayo Kocha Msaidizi wa Yanga,
Charles Boniface Mkwasa, aliyafafanisha na
zawadi, kumekuwapo na maneno
yanayomhusisha kipa Juma Kaseja na mlinzi
Yondani na tuhuma za kucheza chini ya
kiwango.
Friday, April 4, 2014
Beno Njovu:Hafukuzwi mchezaji
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment