TIMU ya Soka ya Taifa ya Tanzania (Taifa
Stars), leo inaikabili Burundi (Intamba
Murugamba) katika mechi ya kimataifa ya
kirafiki kuadhimisha miaka 50 ya Muungano
wa Tanganyika na Zanzibar.
Tanganyika na Zanzibar ziliungana Aprili 26,
1964 na kuunda Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania chini ya waasisi Mwalimu Julius
Nyerere na Shekhe Amri Abeid Karume.
Burundi iliwasili nchini juzi tayari kwa mechi
hiyo itakayoanza saa 10 kamili kwenye Uwanja
wa Taifa, Dar es Salaam na kuchezeshwa na
mwamuzi kutoka Kenya, Anthony Ogwayo.
Taifa Stars imekuwa kambini jijini Dar es
Salaam tangu mwishoni mwa wiki iliyopita,
ikiwa inaundwa na wachezaji wazoefu pamoja
na vijana waliotokana na mchakato uliofanywa
katika mikoa mbalimbali.
Timu hii itawakosa wachezaji wake watatu
wanaocheza soka ya kulipwa ambao ni
Mbwana Samata, Thomas Ulimwengu
wanaochezea TP Mazembe na Mwinyi
Kazimoto anayecheza soka la kulipwa Qatar.
Aidha, mechi hiyo inatarajiwa kushuhudiwa na
kocha mpya wa Stars, Martinus Mart Nooij,
raia wa Uholanzi ambaye anatarajiwa
kuchukua nafasi ya Kim Poulsen aliyefukuzwa
na uongozi mpya wa soka Tanzania.
Akizungumzia mchezo huo, Ofisa Habari wa
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF),
Boniface Wambura aliwataka wananchi
kujitokeza kwa wingi ili kuwaona wachezaji
wapya waliopatikana katika mkakati wa
maalumu wa kupata wachezaji chipukizi wa
timu ya Taifa.
Wambura alisema wachezaji hao
watakaochanganyika na wachezaji wakongwe
wanatarajia kuonesha soka safi baada ya
kukaa kwa muda mrefu katika kambi maalumu
ya mafunzo.
Alisema ni mchezo wa aina yake hasa
ikizingatiwa kuwa timu hizo zote zipo katika
mchakato wa kujiandaa kushiriki kwenye
michuano ya awali ya Kombe la Mataifa ya
Afrika (Afcon).
Alisema ikumbukwe kuwa wachezaji hao
walicheza katika michuano ya Cecafa mwaka
jana ambapo Tanzania ilishinda kwa bao 1-0.
“Huu utakuwa ni mchezo wa aina yake kwa
kuwa wote wapo katika mchakato wa kunoa
vikosi kushiriki kwenye michuano hiyo
muhimu, hivyo basi wachezaji wanakuwa na
hali nzuri ya kimchezo katika kuhakikisha
kuwa wanacheza soka safi na lenge kuvutia,
watu waje kwa wingi kujionea soka hilo,”
alisema.
Wachezaji wa Stars waliopo kambini ni
Deogratias Munishi, Mwadini Ali, Aidan
Michael, Aggrey Morris, Erasto Nyoni, Hassan
Mwasapili, Kelvin Yondani, Said Morad, Amri
Kiemba, Frank Domayo, Himid Mao, Jonas
Mkude, Athanas Mdamu, Haruna Chanongo,
Juma Liuzio, Khamis Mcha, Mrisho Ngasa,
Ramadhan Singano na Simon Msuva.
Wengine ni Benedicto Mlekwa, Emma
Simwanda, Joram Mgeveje, Omari Kindamba,
Edward Mayunga, Shiraz Sozigwa, Yusuf
Mlipili, Said Ally, Abubakar Mohamed, Hashim
Magona, Omari Nyenje, Chunga Zito,
Mohammed Saidi, Ayoub Lipati, Abdulrahman
Ally na Paul Bundara.
Viingilio vya mechi hiyo ni VIP A Sh 20,000,
VIP B na C ni Sh 10,000 na cha chini ni Sh
5,000.
Friday, April 25, 2014
Stars kuminyana na Burundi leo.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment