KOCHA Mkuu wa Manchester United, David
Moyes amefutwa kazi, ikiwa ni miezi 10 tu
baada ya kumrithi Sir Aex Ferguson.
Alitimuliwa baada ya mkutano na Makamu
Mwenyekiti wa klabu hiyo, Ed Woodward katika
uwanja wa mazoezi wa Carrington,
Manchester jana saa mbili asubuhi kwa saa za
Uingereza.
Moyes, 50, alichaguliwa na Ferguson kuwa
mtu wa kumrithi wakati alipostaafu baada ya
miaka 26 ya kuiongoza klabu hiyo ya Old
Trafford mwishoni mwa msimu uliopita.
Kocha mchezaji, Ryan Giggs anatarajiwa
kuiongoza United katika mechi ijayo ya
nyumbani dhidi ya Norwich City, Jumamosi
wiki hii.
Kocha Mholanzi Louis Van Gaal, kocha wa
Borussia Dortmund, Jurgen Klopp, wa Atletico
Madrid, Diego Simeone na yule wa Paris St-
Germain, Laurent Blanc tayari wanatajwa
katika kumrithi Moyes.
Hata hivyo, Klopp ambaye mapema msimu huu
alisaini mkataba mpya hadi mwaka 2018,
amelieleza gazeti la Guardian la Uingereza
kuwa atabaki Signal Iduna Park.
“Man Utd ni klabu kubwa na ninajisikia vizuri
na mashabiki wake wa kuvutia,” alisema
Klopp. “Lakini utiifu wangu kwa Borussia
Dortmund na watu wake hauwezi kuvunjika.”
Aidha, imefahamika kuwa makocha Steve
Round na Jimmy Lumsden pia wameachia
ngazi nafasi zao, lakini kocha wa makipa Chris
Woods na kocha wa timu ya kwanza, Phil
Neville watabaki hadi mwisho wa msimu.
United ilikataa kutoa maoni kuhusu taarifa za
magazeti ya Uingereza juzi kwamba Moyes
ambaye aliondoka Everton na kusaini mkataba
wa miaka sita na mabingwa hao wa Ligi Kuu
ya England, angefukuzwa kabla ya mwishoni
mwa msimu huu. Lakini taarifa ya klabu hiyo
jana ilisema, “tungependa kuweka
kumbukumbu sawa, kwa kutoa shukrani kwa
kujituma kwa bidii, ukweli na uadilifu aliouleta
wakati wa kutekeleza jukumu lake.”
United iliyo katika nafasi ya saba zikiwa
zimebaki mechi nne, imejihakikishia kupata
pointi chache katika Ligi Kuu baada ya
kutaabika hasa Old Trafford msimu huu. Chini
ya Moyes, alipoteza mechi sita nyumbani,
alifungwa na Swansea katika Kombe la FA
kwenye Uwanja wa Old Trafford, na ilishindwa
kuizuia Sunderland kuwatoa katika nusu fainali
ya Kombe la Ligi.
Machi mwaka huu, baadhi ya mashabiki
walikodi ndege na kuruka juu ya uwanja huo
wakati wa mechi yao ya Ligi Kuu dhidi ya
Aston Villa, ikiwa na bango lenye maneno
“Wrong One – Moyes Out” (ikimaanisha
Moyes hakuwa chaguo sahihi na anastahili
kuondoka) – ikiwa ni kama kupingana na
bango jingine uwanjani hapo lililombatiza
Moyes kuwa “Chosen One.”
Mashetani Wekundu hao pia watakosa
kucheza Ligi ya Mabingwa kwa mara ya
kwanza tangu mwaka 1995 na wako katika
hatari ya kukosa kabisa michuano ya Ulaya
kwa mara ya kwanza tangu mwaka 1990.
United ilifuzu kwa robo fainali ya Ligi ya
Mabingwa kabla ya kutolewa na Bayern
Munich na Moyes alidai kuwa kikosi hicho
kilicheza vyema katika michuano hiyo.
Hata hivyo, kumekuwapo na madai kuwa
alikuwa hakubaliki kwa wachezaji wa Man
United, kiasi kwamba kiungo Anderson
alipohamia Fiorentina kwa mkopo Januari,
alidai wachezaji wa timu hiyo wanataka Moyes
aondoke. Baadaye alikanusha kauli hiyo.
Lakini Rio Ferdinand na Robin van Persie pia
wamewahi kukaririwa wakitoa kauli kama hizo,
wakati Javier Hernandez na Wilfried Zaha
wamewahi kuandika katika mitandao ya
Twitter kumkana kocha wao.
Baada ya kipigo Jumapili wiki hii dhidi ya timu
yake ya zamani Everton, ilikuwa dhahiri Moyes
siku zake katika Old Trafford zilikuwa
zinahesabika.
Alijiunga na timu hiyo baada ya misimu 11
katika Everton na alisema asingeweza kukataa
fursa ya kuhamia Old Trafford. Alianza kazi
rasmi Julai mosi.
Anakuwa kocha wa tatu kukaa muda mfupi
katika United, na ni mara ya kwanza tangu
Novemba 6, 1986 kwamba Manchester United
imefukuza kocha.
Moyes, ambaye ni raia wa Scotland,
ameifundisha United mechi 49, akimpiku Walter
Crickmer katika mechi 43 katika kipindi chake
cha kwanza kati ya viwili vya ukocha, wakati
Lal Hilditch ndiye aliyekaa muda mfupi zaidi,
akidumu kwa mechi 33 kati ya Oktoba 1926 na
Aprili 1927.
Tuesday, April 22, 2014
Moyes OUT!!!
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment