WAZIRI Mkuu, Mizengo Pinda amewazawadia
washindi wa Kombe la Dunia la Watoto wa
Mitaani Sh 500,000 kila mchezaji, huku
akiwaongezea kidogo wachezaji watatu
waliong’ara nusu fainali na fainali.
Timu hiyo ya watoto wenye umri chini ya
miaka 16, ilipangwa Kundi la 2 pamoja na
Argentina, Nicaragua, Philippines na Burundi na
kulikuwa na makundi matatu.
Tanzania iliingia nusu fainali kwa kuwa mshindi
wa pili na pia kumenyana na Marekani na
kuichapa mabao 6-1 na baadaye kuitoa
Burundi kwa mabao 3-1.
Pinda alitangaza zawadi hiyo nyumbani kwake
mjini Dodoma jana, alipokutana na washindi
hao kwa chakula cha mchana na kuwapongeza
kwa kuitangaza Tanzania vyema.
“Mmetupa heshima kubwa sana na nimeona
tusiishie kwa kuwaona bali mpitie katika Bunge
Maalumu wajumbe watafurahi kuwaona.
Changamoto mliyotupa ni kubwa sana kwangu
binafsi, kwa viongozi na Wizara,” alisema
Waziri Mkuu Pinda.
Wachezaji walioongezewa kidogo zaidi ya Sh
500,000 ni Kipa Bora, Emmanuel Chaka,
aliyepewa kombe na mfungaji wa mabao
manne katika nusu fainali dhidi ya Marekani,
Michael Simon.
Mwingine aliyeongezewa zawadi ni mfungaji
wa mabao yote matatu ya fainali dhidi ya
Burundi, Frank Willium. Kabla ya kuanza
kuzungumza, Pinda alitoa nafasi kwa mmoja
wa watoto hao, Majuto Ismail, aeleze hali
ilivyokuwa katika michuano hiyo mpaka
wakafikia mafanikio hayo.
Majuto aliyecheza katika michuano iliyopita
Afrika Kusini na kuwa washindi wa pili na
katika michuano hii, alikwenda kama Meneja,
alisema walipofika Brazil katika Jiji la Rio de
Janeiro, walikuwa timu ya sita kufika.
Mashindano yalipoanza alisema walicheza kwa
kujituma na walikuwa na nidhamu nzuri kwa
kufuata sheria, kiasi ambacho kama
kungekuwa na zawadi ya nidhamu
wangepewa.
Baada ya kushinda, Majuto alisema
walikwenda kutembelea vivutio vya Brazil,
ikiwemo wanakoishi watoto wa mazingira
hatarishi.
Majuto aliyesema kuwa hapendi kuitwa mtoto
wa mitaani kwa kuwa mtaa hauzai, alitakiwa
na Pinda kufafanua hilo eneo walilokwenda
linafanana na eneo gani Tanzania, na akajibu
linafanana na Mwanza ambako yeye amekulia
katika mazingira magumu.
Akifafanua kuhusu dhana ya maisha ya watoto
wa mazingira magumu katika nchi
zilizoendelea na nchi masikini, Pinda alisema
hata jina Kombe la Dunia la Watoto wa Mitaani
halipendi, lakini ndivyo linavyoitwa.
Alifafanua kuwa watoto hao ni ambao
hawajakua katika mazingira nadhifu na kupata
mapenzi ya baba na mama. Alisema pamoja na
mazingira hayo, watoto hao wametoa funzo
kuwa hata katika mazingira magumu,
wameonesha karama zao na kuleta heshima
kwa Taifa na kazi iliyopo ni kukuza karama
zao.
“Msikate tamaa kwa kuitwa hivyo, inaonekana
kama vile tusi, lakini ni aina ya uhalisia ambao
mmeutumia kuleta kitu kizuri,” alisema Pinda
na kuongeza kuwa atawasiliana na uongozi wa
Mkoa wa Mwanza wawape mapokezi mazuri
na yeye akitembelea mkoa huo, atakwenda
kuwaona.
Katika hatua nyingine kabla ya kuonana na
Pinda, wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba
waliamua kuchangia timu hiyo ya watoto wa
mitaani.
Makamu Mwenyekiti wa Bunge Maalumu la
Katiba, Samia Suluhu Hassan, alisema jana
wataandaa utaratibu kwa wajumbe wa Bunge
hilo wanaopenda kuwachangia watoto hao
kufanya hivyo.
Alisema hayo alipokuwa akijibu hoja ya
Mbunge wa Viti Maalumu, Diana Chilolo,
aliyeomba wajumbe wa Bunge Maalumu,
wawachangie watoto hao waliopeperusha
vyema Bendera ya Tanzania nchini Brazil.
Watoto hao walifika jana katika Bunge
Maalumu na kutambulishwa kuwa wageni wa
Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na
Michezo, Dk Fenella Mukangara.
Naye Naibu Waziri wa Habari, Vijana,
Utamaduni na Michezo, Juma Nkamia
alifananisha washindi hao na timu ya Mathare
United ya Kenya ambayo iliundwa na watoto
wa mitaani na baadaye kufanikiwa kuchukua
ubingwa wa Afrika Mashariki.
Alisema timu hiyo ilitunzwa na kutoa wachezaji
wazuri akiwemo Victor Wanyama ambaye leo
anacheza katika ligi kubwa duniani, Ligi Kuu ya
England katika klabu ya Southampton.
Katika hatua nyingine, Rais Jakaya Kikwete
ameipongeza timu ya Watoto wa Mitaani ya
Tanzania kwa kutwaa Kombe la Dunia jijini Rio
de Janeiro, Brazil.
“Mmetuwakilisha vyema, ninawapongeza
sana, pia mmewapa moyo watoto wengine
wote wenye vipaji maalumu, lakini
hawakubahatika kuwa na makazi rasmi,
hongereni sana,” alisema Rais Kikwete.
“Hongereni kwa kujituma na kucheza kwa
ustadi,” alisema Rais na kuwaasa watoto hao
“ongezeni bidii, nidhamu na mazoezi ya
kutosha na hakika mtafanikiwa zaidi na
kulibeba jina la Tanzania mbali zaidi ya hapa
katika ulimwengu wa soka duniani, kwani
hakuna kisichowezekana kama mtazingatia
maelekezo, mafunzo, bidii na nidhamu ya yote
mnayofanya.”
Saturday, April 12, 2014
Mabingwa wa kombe la dunia la watoto wa mtaani wazawadiwa fedha
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment