Saturday, February 22, 2014

HATUMTAKI OZIL

MESUT Ozil, staa aliyesajiliwa kwa pesa nyingi
kwenye kikosi cha Arsenal, Jumatano iliyopita
alikosa penalti ya tatu wakati klabu yake
ilipomenyana na Bayern Munich katika mchezo
wa kwanza wa hatua ya mtoano ya Ligi ya
Mabingwa Ulaya uliochezwa uwanjani Emirates.
Kiungo huyo Mjerumani aliangushwa ndani ya
boksi na beki, Jerome Boateng, jambo
lililomfanya mwamuzi aamuru ipigwe penalti.
Lakini staa huyo aliyesajiliwa kwa Pauni 42.5
milioni, alipiga kizembe na  kuupeleka mpira
mikononi mwa kipa, Manuel Neuer,
aliyepangua mkwaju huo.
Neuer alikuwa rafiki wa Ozil walipokuwa shule,
inawezekana kipa huyo anamtambua vizuri
kuhusu upigaji penalti wake ukiweka kando
kwamba wawili hao wamo kwenye kikosi cha
timu ya taifa ya Ujerumani.
Mbovu wa penalti
Supastaa huyo aliyetua Arsenal mwaka jana
akitokea Real Madrid, si mchezaji makini
linapokuja suala la kupiga penalti.
Penalti ya Jumatano iliyopita ilikuwa ya tatu
kwake kukosa kwenye kikosi cha Arsenal katika
Ligi ya Mabingwa Ulaya. Alikosa pia wakati
timu hiyo ilipomenyana na Olympique
Marseille mwanzoni mwa msimu.
Kwenye kipindi cha miaka mitatu aliyodumu na
kikosi cha Real Madrid, Ozil hakuwahi kupewa
penalti apige. Mkwaju mwingine aliowahi
kuukosa ni ule wakati alipokuwa akiichezea
Werder Bremen kwenye mechi dhidi ya
Borussia Monchengladbach mwaka 2009.
Makali ya staa huyo yaliyoanza kwa kasi
mwanzoni mwa msimu,  yamepungua kiasi
kikubwa na hajafunga bao katika mechi 13
zilizopita. Katika mechi 15 ametengeneza nafasi
tatu tu za kufunga.
Mashabiki wamchoka
Ozil ameendelea kucheza kwa kiwango cha
chini dhidi ya klabu kubwa na Jumatano
iliyopita aliendelea kuboronga. Kukosa kwake
umakini ndani ya uwanja, kumeifanya timu
yake kuchapwa 2-0.
Baada ya matokeo hayo na kiwango chake
mchezoni, mtandao wa goal.com, uliibua
mjadala kama kiungo huyo anapaswa kuendelea
kupata namba kwenye kikosi cha kwanza cha
Arsenal au atupwe benchi.

No comments:

Post a Comment