Saturday, February 15, 2014

MAURINHO AIPA NAFASI LIVERPOOL KUTWAA UBINGWA

SIO sisi tu wala Arsenal au Manchester City,
lakini hata Liverpool wana nafasi kubwa ya
kuchukua ubingwa wa Ligi Kuu England msimu
huu. Hiyo ni kauli ya kocha wa Chelsea, Jose
Mourinho, akipima joto la ligi hiyo maarufu
duniani.
Ushindi wa mabao 3-2 wa Liverpool dhidi ya
Fulham wa Jumatano usiku, unaiacha klabu
hiyo ya Merseyside kuwa pointi nne tu nyuma
ya vinara Chelsea huku zikiwa zimesalia mechi
12 kabla ya ligi hiyo kumalizika.
Wakati Chelsea, Arsenal na Manchester City
zikiwa zinakabiliwa na mechi za Ligi ya
Mabingwa Ulaya pia, Liverpool imebakiwa na
michuano ya Kombe la FA tu na ukweli huo
unamfanya Mourinho aamini kuwa hii ni faida
kubwa kwa Liverpool.
“Wakati ninaposema sisi sio watarajiwa
wakubwa wa ubingwa, kila mtu hapa anaanza
kusema kuwa nimeanza tabia yangu ya
kuchezeana akili. Lakini hizo ni hisia zangu tu.
Ligi hii inashangaza sana. Ni ngumu kwa kila
mmoja wetu,” alisema Mourinho.
“Kuna ambazo zina nafasi kubwa kuliko
nyingine. Kwa mfano, kuna Liverpool ambayo
ina nafasi kubwa kwa sababu haichezi katika
Ligi ya Mabingwa. Kucheza katika Ligi ya
Mabingwa kunatumia nguvu nyingi na umakini
kwa timu zilizopo.
“Nadhani itachekesha sana. Tulipoteza pointi
mbili na kupata moja dhidi ya West Brom na
nadhani itakuwa kama hivi mpaka mwishoni
mwa msimu. Kila timu inahitaji pointi kwa
sababu mbalimbali. Wengine ili wasishuke
daraja, wengine kwa ajili ya kucheza Ligi ya
Mabingwa, kwa hiyo pointi zitakuwa ngumu.”
Katika mechi mbili zilizopita, Chelsea
imeambulia pointi nne, wakati Manchester City
na Arsenal zote zimeambulia pointi moja kila
moja na hivyo kufanya mpambano wa timu za
juu kuwa mkali.
Kiungo ambaye pia ni nahodha wa Liverpool,
Steven Gerrard, alikiri kwamba wao wamekuwa
wakiufukuzia ubingwa kimya kimya ingawa ni
mapema kusema lolote kuhusu taji hilo.
“Sisi tunaendelea kucheza na kujaribu kushinda
mechi nyingi kadiri tuwezavyo. Tuna faida kwa
sababu hatuchezi michuano ya Ulaya, tuna Ligi
tu na michuano ya FA ndio ambayo
tunaizingatia kwa umakini,” alisema Gerrard
ambaye penalti yake ya dakika za majeruhi
iliipatia Liverpool ushindi muhimu.

No comments:

Post a Comment