Saturday, February 15, 2014

SABABU ZA MKE WA ROONEY KUMTAKA MUMEWE AENDELEE KUICHEZEA MANCHESTER UNITED NI HIZI HAPA

MREMBO Coleen Rooney anasubiri kwa hamu
kubwa mazungumzo ya mkataba mpya wa
mumewe, Wayne Rooney wa kuendelea kubaki
klabu Manchester United. Taarifa zinabainisha
kwamba mchezaji huyo anaandaliwa mshahara
wa pauni 300,000 kwa wiki.
Mrembo huyo anadaiwa kumtaka mumewe
asaini mkataba mwingine wa miaka mitano wa
kubaki Manchester ili kuwasubiri watoto wao;
Kai, 4, na Klay mwenye umri wa miezi minane
kuwa na umri mkubwa kabla ya kuhama.
Mkataba ambao Manchester United inataka
kumpa Rooney una thamani ya pauni 65
milioni na utamfanya straika huyo kuwa
mchezaji anayelipwa pesa nyingi zaidi England.
Kwa sasa analipwa kiwango sawa na mchezaji
mwenzake wa Manchester United, straika wa
Kidachi, Robin van Persie, pauni 250,000 kwa
wiki.
Rafiki wa mrembo Coleen, 27, anasema: “Kitu
kikubwa Coleen hataki wahame kutoka
Kaskazini Magharibi na jambo hilo ni muhimu
sana kwa Wayne. Hataki kuondoka eneo hilo na
kutokana na kupokea ofa nzuri ya pesa nyingi
anaamini hilo ni jambo muhimu akabaki klabu
hapo.”
Manchester United imeipiga marufuku Chelsea
kwamba isithubutu kumfuatilia straika wao
huyo kwa sababu hawawezi kumuuza kwa
wapinzani. Real Madrid pia inafukuzia saini ya
staa huyo wa Old Trafford.
Lakini, Coleen hayupo tayari kuona watoto
wake wakihamia London wangali wadogo hivyo,
ukiweka kando Hispania. Anachotaka yeye
waendelee kubaki Manchester hadi hapo
baadaye.
Familia hiyo inaishi Prestbury, Cheshire, na
wazazi wa Coleen, Colette na Tony wanaishi
umbali wa maili 50 huko Formby, Merseyside,
karibu na familia ya akina Rooney.
Coleen amesema Rooney, ambaye alijiunga na
Manchester United akitokea Everton mwaka
2004, atapata shida sana kutulia kama atacheza
bila ya sapoti ya familia zao.
Lakini, kuna mtazamo tofauti wakati kocha
David Moyes akihaha na kuafiki mshahara wa
pauni 300,000 kwa Rooney, wachambuzi wa
soka wanadhani Manchester United inapaswa
kulichukulia kwa hadhari suala la mchezaji
huyo.
Staa huyo tayari anaonekana kuiringia
Manchester United kwa kuweka kando suala la
kusaini mkataba mpya akisubiri hatima ya
klabu mwishoni mwa msimu kama itakuwa
ndani ya nne bora na kama klabu hiyo itafanya
usajili wa mastaa wapya.

No comments:

Post a Comment