UCHAGUZI Mkuu wa Yanga umesogezwa
mbele hadi Juni 14 mwakani huku wanachama
wakimtaka Mwenyekiti wao Yusufu Manji
kuwania tena nafasi hiyo kwa kipindi cha
miaka minne au minane endapo itakubaliwa
kwenye Katiba.
Awali, Uchaguzi Mkuu wa Klabu hiyo
ulipangwa kufanyika Juni 15 mwaka huu, lakini
wanachama wa Yanga waliokuwa na mkutano
wa marekebisho ya Katiba jana kwenye
ukumbi wa Polisi Osterbay waliamua uchaguzi
huo usogezwe mbele ili kupisha marekebisho
ya Katiba.
Aidha, wanachama wa klabu hiyo wamepitisha
vipengele viwili vilivyoongezwa kwenye Katiba
yao kimoja kikiwa ni kuunda Kamati ya Maadili
kilichopendekezwa na Shirikisho la Soka
Tanzania (TFF) lakini wakihitaji marekebisho
badala ya Kaimu Mwenyekiti iwe Makamu
Mwenyekiti.
Aidha, wanachama wameipa mamlaka Kamati
ya Utendaji kufanya nyongeza ya mabadiliko
katika Katiba ya Yanga endapo itahitajika na
TFF ndani ya miezi isiyozidi mitatu kuanzia
tarehe ya jana bila kuitisha mkutano wa
wanachama.
Katika mkutano huo, Manji alitangaza kwa
wanachama kuwa hatogombea nafasi hiyo kwa
mara nyingine, jambo ambalo wanachama
hawakukubaliana naye.
Baada ya kauli hiyo, Mwenyekiti wa Baraza la
Wazee la Yanga Jabir Katundu alihoji
wanachama kama wanakubaliana naye, jibu la
hapana likatawala, wakimuomba aendelee na
ndipo akaamua kupisha mjadala dhidi yake
ufanyike kwa haki huku yeye akitoka nje.
Katika mjadala huo ulioongozwa na Mwenyekiti
wa Baraza la Wadhamini wa Yanga Fatuma
Karume na mjumbe Francis Kifukwe
wanachama walikubali kwa pamoja agombee
na ndipo Manji alipoitwa kuelezwa msimamo
wa wanachama.
Wanachama wengi walipendekeza akae
madarakani kati ya miaka minne au minane
baada ya kufanikiwa kurejesha imani ya
wanachama na kuwezesha pia, Yanga
kumaliza Ligi ikiwa na tuzo ya nidhamu.
Kwa mujibu wa Katiba ya Yanga uongozi
unakaa kwa miaka minne kabla ya kufanyika
uchaguzi mkuu, lakini wanachama
wamependekeza muda wa ukomo wa uongozi
uingizwe kwenye Katiba kwamba ni miaka
minane jambo ambalo Manji alisema linatakiwa
kuingizwa kwenye Katiba.
Pia, wanachama hao walipendekeza badala ya
kuitwa Mwenyekiti, awe Rais jambo ambalo
linahitaji kufanyiwa marekebisho ya Katiba
ndipo likubalike.
Baada ya Manji kuitwa kwa ajili ya kukubali
ombi la wanachama hao alisema:
“Siwezi kusema hapana kwa mama wa Taifa
(Fatma ambaye ni mke wa Rais wa Kwanza wa
Zanzibar Abeid Karume), naona aibu
kumkatalia kwa sababu ataona kuwa
nimemdharau, nashukuru kwa imani yenu
kwangu, naomba mnipe muda, uchaguzi
usogezwe mbele kwa mwaka mmoja sababu
ya marekebisho ya Katiba kisha mengine
yafuate,” alisema.
Alisema nia ya kusogeza mbele ni kutoa nafasi
ya katiba hiyo kuingiza baadhi ya
mapendekezo yaliyotolewa na wanachama hao
na kwamba hadi Katiba ikubalike kwa msajili,
uchaguzi utangazwe siku 60 muda utakuwa
umeenda kwani wakati huo atakuwa akihitajika
kocha mpya na timu itakuwa kwenye
maandailizi ya Ligi Kuu.
“Nia ya Yanga ni kufanya vizuri katika
michuano ya kimataifa na Ligi Kuu tunahitaji
maandalizi sasa tukisema tufanye uchaguzi
Septemba mwaka huu tutaipeleka Yanga
pabaya,”alisema na kuongeza kuwa sasa
viongozi watakuwa ni wale wale isipokuwa
Kamati ya Utendaji itabadilishwa.
Katika hatua nyingine, Manji alisema kati ya CV
(wasifu) saba za makocha walizopitia kwa ajili
ya kuifundisha Yanga, wamechagua moja ya
Kocha wa zamani wa Taifa Stars Marcio
Maximo hivyo wanaendelea kufanya naye
mazungumzo.
Pia, alisema katika kukiimarisha kikosi hicho
wataongeza wachezaji wawili wa kigeni na
watatu wa nyumbani lengo ni kufanya vizuri
msimu ujao.
Monday, June 2, 2014
UCHAGUZI YANGA:Sasa ni hadi 14 June mwakani
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment