KAMATI ya Uchaguzi ya klabu ya Simba, chini
ya Mwenyekiti Dk Damas Ndumbaro,
imewaondoa wagombea saba katika
kinyang’anyiro cha kuwania nafasi ya Ujumbe
wa Kamati ya Utendaji wa klabu hiyo, huku
wagombea wengine watano wakitangaza
kujitoa katika mchakato huo kwa sababu za
kifamilia.
Aidha, mbali na kuwaengua wagombea hao,
Ndumbaro alimzungumzia aliyekuwa mgombea
wa nafasi ya Rais wa klabu hiyo Michael
Wambura na kutaka wanachama
wasiyumbishwe na kauli zake.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar
es Salaam jana, Ndumbaro alisema, katika
mchakato mzima wa usaili, kamati yake
iliongozwa na Ibara ya 26, ambako wagombea
wote saba walioenguliwa walibanwa na vifungu
vidogo vya 2 na 6, hivyo kukosa sifa za kubaki
katika uchaguzi huo.
Kwa mujibu wa Ndumbaro, kifungu kidogo cha
2 kinataka mgombea awe na elimu ya kidato
cha nne anayetambuliwa na Baraza la Mitihani
la Taifa, wakati kifungu cha 6 kinataka
mgombea awe na uanachama wa klabu hiyo
usiopungua miaka mitatu na si chini ya hapo.
Ndumbaro aliwataja wagombea waliondolewa
kwa kutokidhi Ibara ya 26 kifungu kidogo cha 2
kuwa ni George Wakuganda na Salim Jazza,
wakati wagombea Ahmed Mlanzi, Emmanuel
Kazimoto, Omary Omary, Ramson Rutiginga na
Selemani Dewji wakishindwa kukidhi Ibara ya
26 kifungu kidogo cha 6.
Aliwataja wagombea waliojitoa katika
kinyang’anyiro hicho kuwa ni Emmanuel
Mayage na Joseph Itang’are ‘Kinesi’
waliokuwa wakiwania nafasi ya Makamu wa
Rais, pamoja na Asha Kigundula, Hussein
Simba na Juma Pinto, waliokuwa wakiwania
nafasi ya Ujumbe wa Kamati ya Utendaji.
“Wagombea waliojitoa, kwetu wameeleza
kufanya hivyo kutokana na sababu za
kifamilia, ambazo kama kamati hatuko huru
kuhoji, zaidi ya kuridhia.Ama kuhusu
waliopitishwa, wapo wanaoweza kuondolewa
kutokana na baadhi ya masuala kufikishwa
mikononi mwa vyombo vya dola,” aliongeza
Ndumbaro.
Alifafanua zaidi Ndumbaro alisema, baadhi ya
wagombea taarifa zao ziko mikononi mwa
vyombo vya dola ambavyo ni Taasisi ya
Kuzuia na Kupambana na Rushwa Tanzania
(Takukuru) na Baraza la Mitihani la Taifa
(Necta), na kwamba watakaokutwa na makosa
wanaweza kuondolewa kwenye mchakato huo.
Akizungumzia tuhuma za rushwa ya ngono na
pesa zilizoelekezwa kwa kamati hiyo na
mgombea Urais waliyemuondoa, Michael
Wambura, Ndumbaro alisema kuwa
amesikitishwa na tuhuma hizo na maneno
mengine machafu yaliyotolewa na Wambura,
aliyemtaja kama bingwa wa soka la
mahakamani.
Kamati hiyo ya Ndumbaro ilimuengua Wambura
kuwania nafasi ya rais kwenye uchaguzi huo
kwa madai ya kuwa si mwanachama halali wa
Simba.
“Wanachama Simba wasiyumbishwe na kauli
za Wambura, Kamati haijamuonea wala
haijapokea rushwa ya ngono na pesa
kupindisha sheria. Huyu ni wa kupuuzwa,
kwani kama angekuwa muelewa, alipaswa
kukata rufaa na sio kupakana matope kwa
tuhuma zisizo na ushahidi,” alisema
Ndumbaro.
Ndumbaro alisisitiza kuwa, katika kanuni za
Fifa, TFF na hata Simba zinakataza soka
kupelekwa katika mahakama za kawaida,
hivyo kitendo alichokuwa amefanya Wambura
hadi kusimamishwa uanachama, kilikuwa
sawa na kifo na wao kama kamati,
walichofanya ni kumzika marehemu ambaye
akiachwa ataoza na kunuka.
Mwenyekiti huyo ambaye pia ni mwanachama
wa Simba alisema Wambura ni tatizo kwenye
soka la Tanzania kutokana na tabia zake za
kupenda kukimbilia Mahakamani mara kwa
mara kitu ambacho ndicho kilichomuua na
ndiyo maana Kamati yake kupitia kanuni
imeamua kummalizia kwa kumzika.
“Mtu huyu mmoja ameshaenguliwa kwenye
chaguzi tatu ikiwemo ule wa TFF na wa Simba
mara mbili huoni kama huyu ni tatizo na
ukitaka kujua kama ni tatizo ndiyo sababu
Jamal Malinzi (Rais wa TFF) hajamteua katika
kamati hata moja kati ya 18
alizoziunda,”alisema Ndumbaro.
Ndumbaro pia alisema hawezi kushindana na
Wambura kwa sababu ni mwanafunzi wake
aliyewahi kumfundisha somo la Sheria Chuo
Kikuu Huria cha Dar es Salaam.
Kwa upande wake, Mjumbe wa Kamati hiyo
Amin Bakhressa, alikiri kushtushwa na madai
yaliyotolewa na Wambura kuwa Kamati yao
imeshiriki kupokea rushwa ya ngono na pesa,
hivyo kumtaka mlalamikaji huyo kuthibitisha
tuhuma kwa kumtaja aliyetoa na kupokea
rushwa hizo miongoni mwao, ili wajiwajibishe.
“Tunamuomba athibitishe, vinginevyo
akanushe kwa uzito ule ule aliotoa, kwani
kimsingi tuhuma hizi zimechafua hali ya hewa
hadi ya kifamilia kwa kutuhusisha na tuhuma
za ngono, ambazo kwa weledi na heshima
walizonazo wajumbe wa kamati hii, hawawezi
kushiriki upuuzi huo hata mara moja,”
alisisitiza Bakhressa.
Monday, June 2, 2014
UCHAGUZI SIMBA:Saba waenguliwa
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment