Saturday, May 10, 2014

Wambura nae yumo,mbio za urais Simba

KUMEKUCHA Simba. Ndivyo unavyoweza
kueleza baada ya jana mmoja wa wanachama
wake maarufu kutangaza kuwania urais katika
Uchaguzi Mkuu wa Juni 29, mwaka huu.
Michael Richard Wambura amesema Jumatatu
ijayo atakwenda katika makao makuu ya
Simba, Mtaa wa Kariakoo, Dar es Salaam
kuchukua fomu ya kuwania nafasi hiyo ya juu
katika uongozi wa klabu hiyo.
“Nimeulizwa sana (na waandishi wa habari)
kama nitawania uongozi katika Uchaguzi Mkuu
ujao. Jibu langu ni ndiyo. Jumatatu ijayo saa
tano asubuhi, nitakwenda kuchukua fomu ya
kuwania Urais wa Simba,” alisema Wambura
alipozungumza na gazeti hili jana.
Kiongozi huyo wa zamani wa soka katika
Simba na Shirikisho la Soka (TFF) wakati huo
Chama cha Soka Tanzania (FAT), alisema
ataeleza sababu za kuwania nafasi hiyo baada
ya kuchukua fomu siku hiyo.
“Nitaeleza sababu za kuwania nafasi hiyo
baada ya kuchukua fomu,” alieleza Wambura.
Uchaguzi Mkuu wa Simba umepangwa
kufanyika Juni 29, mwaka huu na fomu kwa
nafasi mbalimbali za uongozi zilianza kutolewa
jana hadi Mei 14, mwaka huu saa 10 jioni.
Mbali ya Wambura, jina jingine linalotajwa
katika kuwania urais wa Simba ni
mwanachama maarufu katika Kundi la Friends
of Simba, Evans Aveva ambaye anatajwa
kuungwa mkono na kundi hilo.
Wambura, ambaye amewahi kuwa Mjumbe wa
Baraza la Michezo la Taifa (BMT), pia
amewahi kuwa Katibu Mkuu wa FAT na
baadaye TFF, kabla ya kushindwa na Leodegar
Tenga katika Uchaguzi Mkuu wa TFF, mwaka
2005.
Baadaye alikuwa Katibu Mkuu wa Simba. Rais
wa sasa wa Simba, Alhaj Ismail Aden Rage
ametangaza kutowania kiti hicho.
Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Kamati ya
Uchaguzi, Dk Damas Ndumbaro, nafasi
zitakazowaniwa ni Rais, Makamu wa Rais na
wajumbe watano wa Kamati ya Utendaji,
mmoja lazima awe mwanamke.
Kamati hiyo itakutana Mei 17, mwaka huu
kufanya uhakiki wa fomu za wagombea, na
Mei 19 watatangaza majina ya wagombea
walioomba nafasi hizo. Fomu zitatolewa kwa
nafasi ya Rais Sh 500,000, Makamu wa Rais
Sh 300,000 na wajumbe Sh 200,000.
Aidha, Mei 20 hadi 22, itakuwa ni siku ya
pingamizi dhidi ya wagombea na wanaotakiwa
kuweka pingamizi ni lazima wawe wanachama
wa klabu hiyo.
Mei 25 wataanza kusikiliza pingamizi, Mei 27
kutoa uamuzi, Mei 29, usaili wa wagombea na
Mei 30, itakuwa ni siku ya kutangaza matokeo
ya usaili.
Kuanzia Juni 2 hadi 9, Kamati ya Maadili na
wadau wataangalia masuala ya kimaadili na
Kamati ya Rufaa itakuwa inasikiliza rufaa
wakati maamuzi yote yatakuwa Juni 10 hadi 12
na kusikiliza rufaa hizo ni Juni 8-12.
Juni 13 hadi 15, itakuwa ni kukata rufaa Kamati
ya Rufaa ya Maadili, na Juni 16-20 kusikiliza
rufaa hizo, wakati Juni 21-23 maamuzi ya
mwisho ya kamati hiyo na siku inayofuata
orodha ya mwisho ya wagombea itatangazwa,
kabla ya kuanza kampeni kuanzia Juni 24 hadi
28.

No comments:

Post a Comment