Saturday, May 10, 2014

Ngorongoro kukipiga na Nigeria leo

TIMU ya soka ya vijana chini ya umri wa
miaka 20 ‘Ngorongoro Heroes’ leo itakuwa
kwenye Uwanja wa Taifa Dar es Salaam
kumenyana na wenzano wa Nigeria katika
mechi ya raundi ya pili ya kuwania kucheza
michuano ya Mataifa Afrika kwa vijana wa umri
huo.
Ngorongoro imefuzu raundi hiyo baada ya
kuiondosha Kenya kwa mikwaju ya penalti.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka Shirikisho la
Soka Tanzania (TFF) mechi hiyo itaanza saa
kumi jioni.
Akizungumzia mechi hiyo, kocha wa
Ngorongoro Heroes John Simkoko alisema
anaamini atapata matokeo mazuri leo licha ya
kukiri kuwa mechi hiyo ni ngumu.
“Nigeria tunawajua ni wazuri lakini hata sisi
pia tuna timu nzuri na tumejiandaa kukabiliana
nao,” alisema Simkoko.
“Nimekaa kambini na wachezaji wangu na
kwenye mazoezi nawaona wanavyofuata
maelekezo yangu, naamini hatutawaangusha
kesho (leo),” alisema.
Fainali za 19 za Mataifa Afrika, zimepangwa
kufanyika Senegal mwakani ambapo
zitashirikisha timu saba zitakazofuzu kwenye
mechi za mchujo kabla ya kuungana na
wenyeji Senegal watakaofanya jumla ya timu
nane kwenye michuano hiyo.
Tanzania haijawahi kufuzu michuano hiyo
tangu ilipofanya hivyo mwaka 1980 ambapo
timu ya wakubwa ilifuzu katika michuano
iliyofanyika Lagos, hata hivyo iliishia kwenye
makundi.
Viingilio katika mechi hiyo ni Sh 2,000 kwa
sehemu zote wakati upande wa VIP itakuwa
Sh 5,000. Kwa mujibu wa TFF, tiketi zitaanza
kuuzwa leo asubuhi kwenye magari maalumu.

No comments:

Post a Comment